
Huwa ni furaha kubwa katika familia mtoto anapozaliwa, na hata katika
tamaduni fulani fulani sherehe kubwa hufanyika kumkaribisha mwanafamilia mpya
aliyezaliwa. Lakini pamoja na familia kuwa katika hali ya furaha, wazazi wa
mtoto aliyezaliwa huwa na maswali mengi ya kujiuliza. Tutamleaje mtoto ili awe
mwanajamii mwenye tabia njema? Lishe ya mtoto wetu iweje ili akue akiwa mwenye
afya njema ya mwili na akili? Tutamwepushaje mwanetu na maradhi haya
yanayotishia maisha ya watoto?. Katika hali ya kutafuta majibu ya maswali haya,
wazazi hujikuta katika kila aina ya sintofahamu
kutokana na ushauri mbalimbali waupatao kuhusu lishe au malezi ya watoto wao.
kutokana na ushauri mbalimbali waupatao kuhusu lishe au malezi ya watoto wao.
Sayansi ya afya inatoa ushauri
ambao utasaidia wazazi wapya kuwa na mwanzo mzuri wa lishe ya mtoto ili
akue akiwa na afya njema. Katika maisha, jinsi vile tunavyoanza, yaweza
kutabiri jinsi vile tutakavyomaliza. Hii inaamaanisha kuwa lishe bora kwa mtoto
katika nyakati zake za mwanzo wa maisha yake, ni muhimu sana kwa afya ya baadae
katika maisha yake. Tafiti zinaonyesha kuwa, lishe bora kwa binadamu katika
utoto wake, huchangia sana kuwa na maisha mazuri baadae, kufanya vizuri
shuleni, kazini na hata jinsi anavyoweza kushirikiana na jamii inayomzunguka.
Pia aina bora ya vyakula tutakavyokula tukiwa wachanga, vitatusaidia baadae
maishani kuwa na miili yenye nguvu na afya, kinga ya mwili iliyo imara na kuwa
na umri mrefu wa kuishi.
Chakula muhimu sana kwa mtoto mchanga katika miezi sita ya mwanzo ya
maisha yake ni maziwa ya mama. Maziwa ya mama ni yenye lishe ya hali ya juu,
yenye mchanganyiko maalum wa virutubisho na kinga kutoka kwa mama kwa ajili ya
mtoto.Vitu muhimu vilivyomo katika maziwa haya ni kinga ya mwili(antibodies), vijidawa (antimicrobial factors), vimeng’enyo,
vitamini, madini muhimu, mafuta na protini (vyote hivi husaidia ukuaji wa
haraka wa mwili na ubongo wa mtoto).
Watoto huanzishiwa lishe ya vyakula vingine wanapokua na umri wa
angalau miezi 4 hadi 6, kwa kuwa watoto wachanga huwa hawawezi kumeng’enya aina
nyingi za vyakula. Kwa kawaida watoto huanzishiwa vyakula hivi pale uzito wao
wa mwili unakuwa mara mbili ya uzito waliozaliwa nao, na hii ni endapo wanaweza
kukaa, shingo imekuwa na nguvu, wanaweza kufungua mdomo wanapopewa chakula na
wanaweza kumeza vyakula laini, mara nyingi huweza kufanya hayo yote wakiwa na
miezi sita.
Vyakula hivi wanavyoanzishiwa watoto huwa ni nyongeza ya maziwa ya
mama na siyo mbadala wa maziwa ya mama. Chakula cha mwanzo cha mtoto ni lazima kiwe cha maji
maji na laini.Pata msaada wa kujua ni wakati gani hasa wa kumuanzishia mtoto
vyakula, wasiliana na wataalamu au wauguzi katika cliniki mtoto anayoudumiwa.
Usimwanzishie mtoto aina nyingi za vyakula kwa wakati mmoja ila umwanzishie
chakula kimoja hadi kingine kwa nyakati tofauti na uchunguze endapo kama kuna
chakula chenye kumletea mtoto aleji. Usimwanzishie mtoto vyakula kama mayai,
asali, karanga au siagi ya karanga na aina nyinginezo na nati kwa sababu
vyakula hivi ni rahisi kusababisha aleji, asali yaweza kuwa na vijimelea vya
bakteria vilivyolala( kwa kitaalam hujulikana kama endospores) ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi kwa watoto
wachanga kwa kuwa kinga yao ya mwili bado haijaimarika.
Tunapowaanzishia vyakula watoto
wachanga, lazima tufuate mtiririko ufuatao; hatua ya kwanza ni kuanza na
vyakula vya nafaka kama uji wa mchele au mahindi. Vyakula hivi huendana na
mwili wa mtoto na ni nadra sana mtoto kuwa na aleji ya vyakula hivi.
Hatua ya pili ni kumuanzishia mtoto vyakula vya mboga mboga.Vyakula hivi
huwa na virutubisho vingi zaidi ya matunda yenye sukari nyingi. Vyakula hivi
vya mboga mboga ni kama viazi vitamu, bitiruti,maboga na karoti ambavyo ni
rahisi kupika na kuviponda ponda kutengeneza chakula laini cha mtoto.
Hatua ya tatu ni kuanza kumpa mtoto vyakula kutokana na matunda. Watoto
wanaoanzishiwa matunda kabla ya kuanzishiwa mboga mboga, hujijenga katika akili
yao kuwa vyakula ni vyenye ladha ya sukari na wanapoanzishiwa mboga mboga
itakuwa vigumu kwao kuzoea ladha yake. Sababu nyingine ni kwamba wanakuwa bado
hawana uwezo wa kumeng’enya sukari iliyo
katika matunda aina ya fructose ipasavyo.Unaweza
kumuanzishia matunda kwa kumpa ndizi mbivu iliyopondwa pondwa na kumchanganyia
na maziwa ya mama. Waweza kumpa pia matunda yaliyopikwa kama tipisi, peasi au
epo.
Hatua ya nne ni kumuanzishia mtoto vyakula vya protini.Vyakula hivi ni
kama maharagwe yaliyopondwa pondwa pia dengu, njegere za kijani na nyama
iliyosagwa. Kwa kuwa tumbo la mtoto linakuwa bado halijaweza kumeng’enya
vyakula hivi vizuri, waweza kuviona vikitoka katika choo cha mtoto vikiwa kama
alivyokula. Hii inapotokea usiwe na wasiwasi, kwa kuwa hali hiyo itatoweka
kadri mtoto anavyoendelea kuvizoea vyakula hivyo.
Watoto zaidi ya mwaka 1 zingatia
mlo kamili wenye makundi yote ya chakula. Mtoto anapokula aina tofauti za
vyakula hukamilisha mlo kamili. Mlo kamili utamsaidia mwanao kupata aina zote
za virutubisho anavyovihitaji. Kuwa mbunifu ili kugundua aina ya chakula mtoto akipendacho.Wakati
mwingine watoto wanapopewa chakula kwa mara ya kwanza huwawia vigumu kuikubali
ladha ya chakula hicho, lakini baada ya muda fulani tunapoendelea kuwapa
chakula hiki hujifunza na kujikuta wamezoea ladha ya chakula hicho. Kama mtoto
hatopenda kula yai la kuchemsha jaribu kumpa maziwa, na kuendelea kubadili
vyakula kadiri mtoto anavyopendelea. Ubunifu wa aina za chakula na ubadilishaji
kulingana na chakula akipendacho, utaondoa tatizo la mtoto kukataa kula. Mfano,
chakula kama nyama kitamwongezea mtoto protini, lakini anaweza pia kupata
protini kutoka katika nati, maharagwe,dengu na njegere.
Ili kumsaidia mtoto aondokane na tatizo la kukataa kula, mpe aina
mbali mbali za vyakula kutoka katika makundi yafuatayo.
Vyakula vya wanga
- Viazi mviringo au viazi vitamu.
- Nafaka kama mahindi, mchele, ngano na nyinginezo.
- Majimbi na ndizi.
Nafaka zisizokobolewa huwa na kiasi kikubwa cha fiba ambazo zina aina
nyingi za virutubisho.Kuwa makini na kiasi unachompa mtoto kwa kuwa nafaka hizi
zisizokobolewa hushibisha sana na kumpa kwa wingi kutasababisha mtoto kuvikataa
vyakula hivi. Kumbuka tumbo la mtoto ni dogo na ni kiasi kidogo kitakachomfanya
ashibe.
Vyakula vyenye kiwango kikubwa
cha madini ya chuma na protini.
Mtoto anahitajika kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya
chuma na protini mara mbili kwa siku.Vyakula hivi ni kama:
- Nyama.
- Samaki.
- Nati.
- Mayai.
- Njegere,maharagwe na dengu.
Hakikisha unanunua nyama yenye
ubora kutoka katika bucha zenye nyama iliyopimwa.Epuka kununua nyama kutoka
wauzaji wa mitaani ili kumwepusha mtoto na magonjwa hususani ugonjwa hatari
kama kimeta. Kama utapendelea kumpa
mtoto vyakula aina ya nati(karanga,kweme,korosho,nazi na nyinginezo) hakikisha
zimesagwa na kumchanganyia katika chakula chake ili kuepuka mtoto kukabwa.
Vyakula kutokana na maziwa.
- Maziwa.
- Jibini.
- Mtindi (yoghurt)
Kama utapenda kumpa mtoto mtindi, chagua ule usiowekewa ladha na usio na
sukari nyingi. Kama utapenda kuongeza ladha, fanya hivyo kwa
kuchanganya na
matunda yenye ladha azipendazo mtoto. Maziwa ni chanzo kizuri cha madini
ya
kalshamu (calcium). Hakikisha mtoto
wako anapata kiasi cha nusu lita ya maziwa kwa siku. Madini haya ni muhimu kwa
kuwa huimarisha mifupa,meno na muhimu kwa utendaji kazi wa misuli. Watoto wenye
upungufu wa madini haya hupatwa na ugonjwa ujulikanao kama rickets ambao husababisha udhaifu wa mifupa ambayo hupinda na
kusababisha matege. Hakikisha mtoto wako anatumia maziwa yasiyoondolewa siagi
kwa kuwa watoto wanahitaji nishati nyingi ya mwili ili wakue. Pia maziwa haya
yasiyoondolewa siagi huwa na kiwango kikubwa cha Vitamini A.
Matunda na mboga za majani.
- Embe,chungwa ,zabibu na nanasi.
- Tikiti maji.
- Parachichi.
- Papai.
- Karoti.
- Mboga za majani.
Matunda ni muhimu kwa watoto kwa kuwa huwaongezea aina mbalimbali za
vitamini muhimu zinazohitajika mwilini. Jaribu kubadilisha aina za matunda
kulingana na ladha aipendayo mtoto.
Vyakula vinavyohitajika kwa
kiasi.
Vyakula vyenye mafuta mengi na sukari nyingi ni kama siagi, mafuta ya
mimea, keki,chokleti,chipsi, biskuti, pipi na vinywaji kama soda.Miili ya
watoto huitaji kiasi kikubwa cha nishati, lakini kuwapa kiasi kikubwa cha
vyakula hivi kwaweza kusababisha kuwa na uzito mkubwa(obesity). Endapo utachagua kumpa vyakula hivi, hakikisha anakula
kiasi kidogo na ikiwezekana ale vyakula hivi kwa vipindi mfano wakati wa sikuu
ya kuzaliwa au siku za mwisho wa wiki pekee.Ni vizuri tahadhari kuchukuliwa kwa
kuwa vyakula vyenye sukari nyingi huweza pia kusababisha magonjwa ya kuoza kwa
meno.
Watoto hawaitaji kula vyakula vyenye chumvi nyingi. Epuka vyakula vya
migahawani ambavyo huwa na chumvi nyingi.
0 comments:
Post a Comment